Rais William Ruto ametoa wito kwa viongozi kushiriki siasa za amani.
Amesema siasa za vurugu na uharibifu wa mali zimepitwa na wakati.
Aidha amesisitiza kuwa wakati wa ushindani wa kisiasa umepita.
“Lazima tukubali kuwa mawazo na masuala yenye tija yanapaswa kuwa msingi wa siasa zetu. Siyo kupotea kwa maisha,” alisema Rais Ruto aliyeanza ziara ya siku tano katikaa eneo la Pwani leo Alhamisi.
Kiongozi wa nchi aliwataka polisi kudumisha sheria ipasavyo kwa mujibu wa katiba.
“Usalama wa nchi yetu si suala la kujadiliwa.”
Alitoa kauli hizo wakati wa ufunguzii wa Ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Lamu katika eneo la Mokowe.
Kadhalika alitoa hundi kwa jamii ya uvuvi ya eneo hilo.
Mawaziri Kindiki Kithure wa Usalama wa Taifa, Aisha Jumwa wa Utumishi wa Umma na Salim Mvury wa Madini pamoja na Gavana wa Lamu Issa Timamy ni miongoni mwa waliokuwapo.
Rais Ruto alionya kuwa serikali itawachukua hatua kali wazazi watakaokosa kuwapeleka watoto wao shuleni.
Alisema serikali imewekeza vilivyo katika elimu kuhakikisha kila Mkenya ana fursa sawa ya kupata elimu.
“Elimu ni lazima. Ni hatia kumweka mtoto nyumbani wakati akiwa ametimiza umri wa kwenda shhuleni,” alisema Rais Ruto.
Waziri Kindiki aliwahakikishia Wakenya kwamba serikali itawalinda pamoja na mali yao dhidi ya wale wanaotaka kuendeleza ajenda yao ya kisiasa.
“Hatutakubali mtu yeyote nchini kutumia visivyo katiba kuwadhuru wengine na kuharibu mali,” alionya Kindiki ikiwa ni dhahiri matamshi yake yaliulenga muungano wa Azimio.
Watu kadhaa walifariki na wengine kujeruhiwa wakati wa maandamano yaliyoitishwa na muungano huo wiki mbili zilizopita.
Azimio inawanyoshea polisi kidole cha lawama kufuatia maafa hayo, madai ambayo serikali imeyapuuzilia mbali.
Gavana Timamy alisema watu wa kaunti ya Lamu hawakushiriki maandamano ya upinzani akiongeza kuwa hiyo siyo “njia sahihi ya kuangazia gharama ya juu ya maisha”.