Umoja wa Mataifa (UN) umesema kuwa zaidi ya wafungwa 100 wa kike walibakwa na kuteketezwa wakiwa hai, wakati wafungwa walipotoroka gereza moja mjini wa Goma, katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mamia ya wafungwa walitoroka katika gereza la Munzenze siku ya Jumatatu, baada ya wapiganaji wa kundi la M23 kuuteka mji huo.
Duru za umoja huo zilisema kuwa kati ya wanawake 165 na 167 walivamiwa na kunyanyaswa na wafungwa wa kiume walipovunja gereza.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wengi wa wanawake hao waliuawa baada ya wafungwa hao kuteketeza gereza hilo.
Goma, jiji kubwa lenye zaidi ya watu milioni moja, lilitekwa baada ya kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kuingia na kuteka eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Jiji hilo lilikumbwa na machafuko huku miili ikiwa imetapakaa mitaani na makombora yakiripotiwa kuonekana juu ya nyumba za makazi.
Picha za jela kuvunjwa za wiki iliyopita zilionyesha watu wakitoroka kutoka kwa jengo hilo huku moshi ukiendelea kufuka kwa nyuma.