Takriban wanariadha 500 watashiriki mbio za kitaifa za nchi Jumamosi hii, Februari 8 katika uwanja wa Eldoret Sports Club.
Washiriki ni wa kutoka matawi 16 yaliyo chini ya chama cha Riadha Kenya, ikiwemo Idara ya Polisi, Magereza, Jeshi, KWS, vyuo vikuu na maeneo mengine 11 nchini.
Mbio hizo kwa mara ya kwanza zitaandaliwa kuanzia saa nane adhuhuri na wala sio asubuhi kama ambavyo imekuwa desturi.
Wanariadha watashindania ubingwa wa kitaifa katika vitengo vya kilomita 10 wanaume na wanawake, kilomita 8 na kilomita 6 kwa vijana chini ya umri wa miaka 18, na kilomita mbili kwa wanaume na wanawake.
Washindi wa kilomita nane watatuzwa shilingi laki mbili, nafasi ya pili 130,000 na shilingi laki moja kwa watakaomaliza nafasi ya tatu.
Washindi wa vijana chini ya umri wa miaka 20 watatunukiwa shilingi 140,000, nafasi ya pili 90,000 na nambari tatu 70,000.
Washindi wa kiliomita mbili watapokea zawadi ya shilingi 50,000, nafasi ya pili 40,000, na nambari tatu 30,000.