Wahudumu wa afya hospitali ya KUTRRH wagoma, shughuli zatatizika

Wahudumu hao wanalalamikia, miongoni mwa mambo mengine, unyanyasaji wa kingono, kufanya kazi kwa saa nyingi na kuondolewa kwa malipo ya matibabu ya wahudumu wanaofanya kazi katika idara zinazotoa huduma muhimu.

Martin Mwanje
2 Min Read

Huduma katika Hospitali ya Mafunzo, Utafiti na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta, KUTRRH zilikwama le o Jumatatu baada ya wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine kufanya mgomo kulalamikia mazingira mabovu ya utendakazi. 

Wote hao wanaitaka Wizara ya Afya kuingilia kati haraka iwezekanavyo na kuangazia malalamishi yao ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono, kufanya kazi kwa saa nyingi na kuondolewa kwa malipo ya matibabu ya wahudumu wanaofanya kazi katika idara zinazotoa huduma muhimu.

Mgomo huo ulikuwa mwiba kwa mamia ya wagonjwa waliokosa matibabu kwenye wodi wakati wafanyakazi hao wakifanya maandamano kwenye ua wa hospitali hiyo.

Wafanyakazi hao pia wamelalamikia hatua ya hivi maajuzi ya kumsimamia kazi Afisa Mkuu wa hospitali hiyo Ahmed Dagane aliyetakiwa na bodi ya hospitali kwenda kwenye likizo ya lazima. Dkt. Isaac Kamau ameteuliwa kukaimu wadhifa huo.

Bodi ya hospitali hiyo ikiongozwa na Prof. Olive Mugenda ilimtaka Dagane kwenda kwenye likizo ya lazima hadi uchunguzi juu ya madai ya matumizi mabaya ya fedha utakapokamilika.

Hatua za wanachama wa usimamizi wa hospitali hiyo kuwahutubia wanahabari zilitibuliwa na wahudumu hao.

Chama cha Madaktari, KMPDU na kile cha wauguzi, KNUN vimeupatia usimamizi wa hospitali hiyo saa 24 kuangazia maalamishi yao la sivyo wasambaratishe kabisa utoaji huduma kwenye hospitali hiyo.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *