Wahadhiri waikosoa serikali juu ya utekelezaji wa CBC

Martin Mwanje & Carolyn Necheza
2 Min Read

Wahadhiri wa vyuo vikuu wameikosoa serikali kuhusu utekelezaji wa mfumo wa umilisi (CBC) wakisema kuwa mipango ya Wizara ya Elimu na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) haijazingatia kikamilifu elimu ya juu.

Wanasema mjadala kuhusu CBC haujajumuisha mpango wa kuwaandaa wanafunzi wa darasa la 9 kwa ajili ya kujiunga na vyuo vikuu.

Kaimu Naibu Makamu wa Chansela wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro, anayesimamia mipango, utafiti na ubunifu, Prof. Peter Bukhala, amesema kuwa mtaala wa CBC haujaunganishwa na elimu ya vyuo vikuu, hali inayoweza kulemaza mfumo mzima wa elimu humu nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Bukhala, wanafunzi wa CBC wanatarajiwa kujiunga na vyuo vikuu mwaka 2029, lakini Wizara ya Elimu haijatoa mwongozo wa jinsi mfumo huo utapanuliwa hadi elimu ya juu.

Wahadhiri sasa wanataka mazungumzo ya mageuzi ya elimu kupanuliwa ili kushughulikia maandalizi ya vyuo vikuu, kuhakikisha kuna mifumo thabiti ya kuwaingiza wanafunzi na kusaidia walimu wa madarasa ya 7, 8, na 9 kukabiliana na changamoto za CBC.

Mfumo wa CBC umekabiliwa na mawimbi ya changamoto tangu kuasisiwa kwake huku wengi wakielezea ukosefu wa miundombinu na walimu wenye ujuzi unaohitajika ili kuutekeleza ipasavyo.

Serikali imesema inaangazia utendakazi wa mfumo huo kwa lengo la kuziba mianya iliyojitokeza na kuuboresha zaidi.

Martin Mwanje & Carolyn Necheza
+ posts
Share This Article