Wahadhiri, wafanyakazi wa vyuo vikuu waapa kuendelea na mgomo

Mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma ulianza Septemba 17 na wameapa kutorejea kazini hadi walipwe malimbikizi yao ya shilingi bilioni 7.9.

Martin Mwanje
2 Min Read
Viongozi wa UASU na KUSU walipokutana na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang'ula Septemba 25

Mgomo wa wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma uliingia siku ya ya nane leo Jumatano huku wakiapa kwamba kamwe hawatarejea kazini hadi serikali itimize matakwa yao. 

Wanataka serikali kuwalipa malimbikizi yao ya kima cha shilingi bilioni 7.9.

Leo Jumatanao, waliandamana hadi makao makuu ya Wizara ya Elimu, Wizara ya Fedha na katika majengo ya bunge ili kushinikiza matakwa yao.

Katika majengo ya bunge, viongozi hao, wakiongozwa na Dkt. Constantine Wasonga wa chama cha UASU na Dkt. Charles Mukhwaya wa chama cha KUSU walikutana na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na kuwasilisha malalamishi yao.

Wetang’ula aliahidi kuwa bunge litaangazia malalamishi yao na kuwaita maafisa wa Wizara ya Elimu akiwemo Waziri Julius Ogamba kuelezea wanachokifanya kusuluhisha mzozo huo.

Kulingana na wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu, serikali imeshindwa kutekeleza Mikataba ya Maelewano (MoU) ya awali na isitoshe mazungumzo ya kufikia MoU ya mwaka 2025-2029 bado hayajang’oa nanga.

Wakionekana kutoyumba katika msimamo wao, wamemnyoshea Waziri  Ogamba kidole cha lawama kwa kuwanyea mvua ya vitisho badala ya kukumbatia ari ya mazungumzo katika kumaliza mgomo wao ulioanza Septemba 17.

Mgomo huo umeathiri masomo katika vyuo vikuu vya umma huku wanafunzi wakiwa hawana budi ila kujisomea na wengine kupata fursa ya kuendeleza shughuli zao za hapa na pale.

Website |  + posts
Share This Article