Wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma waanza mgomo

Martin Mwanje
1 Min Read

Shughuli za masomo zilitatizika leo Jumatano baada ya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma nchini kuanza mgomo wao. 

Wote hao wanalalamikia kucheleweshwa kwa mishahara na yao na kutaka kupatiwa bima ya afya kama ilivyoratibiwa kwenye Mkataba wa Maelewano wa mwaka 2021-2025.

Katika maeneo kadhaa nchini, wahadhiri na wafanyakazi hao waliandamana barabarani na kusikika wakiapa kuwa kamwe hawaterejea kazini hadi matakwa yao yashughulikiwe.

Maandamano ya wahadhiri na wafanyakazi yalishuhudiwa katika vyuo vikuu vya Meru, Maasai Mara na JKUAT.

Katika Chuo Kikuu cha JKUAT, wafanyakazi wapatao 2,000 walisusia kazi wakilalamikia hatua ya usimamizi wa chuo hicho kutowaongezea mshahara.

Wakiongozwa na viongozi wa chama cha wahadhiri (UASU) na kile cha wafanyakazi (KUSU), wafanyakazi hao walitoa wito kwa uongozi wa chuo hicho kukifunga kwani hakuna masomo yataendelea hadi matakwa yao yatimizwe.

Wafanyakazi hao wanataka mkataba wa maelewano (CBA) wa mwaka 2021/2025 utekelezwe wakilalama kuwa utekelezaji wake tayari umekawia kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Miongoni mwa mambo mengine, mkataba huo unaangazia kuongezwa kwa mishahara yao na kuwasilishwa kwa makato yao kwa taasisi husika bila kukawia.

Taarifa zaidi zimetolewa na waandishi wetu Anthony Kioko, Jeff Mwangi na Stanley Mbugua   

Share This Article