Mhubiri Gilbert Deya amefariki kwenye ajali ya barabarani iliyotokea Jumanne eneo la Namba Kapiyo katika baraara kuu ya Kisumu–Bondo.
Kulingana na Afisa Mkuu wa Trafiki eneo la Nyanza Peter Maina, ajali hiyo ilihusisha magari matatu, Toyota Noah iliyokuwa ikiendeshwa na Deya, basi la Chuo Kikuu cha Moi na gari inayomilikiwa na serikali ya kaunti ya Siaya.
Taarifa ya awali ya polisi ilisema kuwa huenda Deya alipoteza mwelekeo na kuingia kwenye safu ya basi ya Chuo kikuu cha Moi. Katika juhudi za kuepuka kugongana ana kwa ana, basi hilo lilianguka na kupinduka, huku gari la Deya likigongana na gari la serikali ya kaunti ya Siaya.
“Deya alifariki papo hapo huku abiria wawili kwenye gari lake, mke wake na mwanamke mwingine wakipata majeraha madogo.
“Mwili wa Deya ulipelekewa katika chumba cha wafu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kombewa Sub-County Hospital mortuary,” alithibitisha Maina, aliyezungumza na mwanahabari wa KBC Wycliffe Oketch mjini Kisumu Jumanne jioni.
Aidha afisa huyo wa trafiki alithibitisha kuwa wanafunzi 13 kwenye basi lhilo la Chuo Kikuu walipata majeraha mabaya, ambapo watatu walipelekwa katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Jaramogi Oginga, huku wengine wakitibiwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kombewa.
Alidokeza kuwa polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo.