Wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma wasitisha mgomo

Hata hivyo, KUDHEIHA  imeapa kurejelea mgomo kuanzia tarehe 6 mwezi ujao endapo serikali haitawalipa wafanyakazi ifikiapo mwishoni mwa mwezi huu.

Dismas Otuke
1 Min Read

Wafanyakazi wa vyuo vikuu vya umma nchini wamesitisha mgomo wa kitaifa uliodumu kwa siku mbili baada ya kuafikiana na serikali.

Akiwahutubia wanahabari siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi wa nyumbani, wahudumu wa mikahawa na vyuo (KUDHEIHA) Albert Njeru, amewataka wanachama wake zaidi ya 12,000 humu nchini kurejea kazini Jumatatu ijayo.

Kulingana na Njeru, Waziri wa Elimu Julius Ogamba ameahidi kuwa shilingi bilioni 2.73, ambazo wafanyakazi wa KUDHEIHA wanadai kupitia malimbikizi ya mishahara na marupurupu katika maafikiano ya nyongeza ya mishahara ya mwaka 2021-2025, zitalipwa pamoja na mishahara ya mwisho wa mwezi huu wa Septemba.

‘Tumeshauriana na serikali na imekubali kulipa shilingi bilioni 2.73 tunazodai ifikiapo mwishoni mwa mwezi huu. Kufuatia hatua hii, nawataka wafanyakazi warejee mahali pao pa kufanya kazi ili kutoa nafasi kwa mazungumzo,”alisema Njeru.

Aidha, Njeru ameongeza kuwa wamepokea agizo la mahakama la kuwataka wasitishe mgomo kusubiri uamuzi wa kesi inayotarajiwa kutolewa Oktoba 15.

Hata hivyo, KUDHEIHA  imeapa kurejelea mgomo kuanzia tarehe 6 mwezi ujao endapo serikali haitawalipa wafanyakazi ifikiapo mwishoni mwa mwezi huu.

 

Website |  + posts
Share This Article