Wabunge siku ya Jumatano, wamekashifu vikali kisa cha kushambuliwa kwa mwakilishi wanawake wa kaunti ya Kirinyaga Jane Njeri Maina.
Maina, ambaye alikuwa akitembea kwa miguu alishambuliwa na kundi la watu waliokuwa wakimzuia kuwahutubia wakazi.
Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wa, aliwaambia wabunge kuwa Njeri yuko katika hali dhabiti baada ya kupokea matibabu hospitalini.
“Nimearifiwa kuwa yuko katika hali dhabiti na tunamtakia afueni ya haraka. Ninatumai maafisa wa polisi wataharakisha kuwatia nguvuni waliomshambulia,”alisema Ichung’wa.
Kwa upande wake kiongozi wa wachache katika bunge la taifa Opiyo Wandayi, alisema uchunguzi wa polisi haupaswi kuwa tu kwa waliomshambulia Njeri, lakini pia waliowafadhili washambulizi hao.
“Ghasia kwa vyovyote vile lazima vikashifiwe. Tunataka wale wote waliohusika kuchukuliwa hatua na idara ya upelelezi wa maswala ya jinai na kuandikisha taarifa na wafikishwe mahakamai,”alisema Wandayi.
Wabunge wengine waliozungumza walilaani shambulizi hilo, wakidokeza kuwa mbunge huyo ni miongoni mwa wabunge wachapakazi zaidi katika bunge la taifa.