Gavana wa kaunti ya Murang’a Irungu Kang’ata ameagiza wasimamizi wote watano wa hospitali za umma katika kaunti hiyo wajiuzulu katika muda wa wiki mbili zijazo kutoa fursa ya kuajiri upya.
Wasimamizi wa hospitali za Murang’a, Maragua, Kirwara, Muriranja na Kangema wana muda hadi Septemba 7 2023, kuondoka kwenye nyadhifa zao.
Kang’ata anasema serikali ya kaunti itatangaza nafasi hizo kwa wanaozitaka kutuma maombi na watakaohitimu, watachaguliwa kuhudumu.
Alielezea kwamba kuanzia sasa wasimamizi wa hospitali watahudumu kwa muda wa mwaka mmoja kukiwa na uwezekano wa kuanzisha tena kandarasi zao.
“Wakati wa kuanzisha upya kandarasi, utafiti unaohusisha wananchi utatekelezwa ili kuamua iwapo afisa anastahili kupatiwa kandarasi nyingine.” alisema Irungu.
Gavana alisema kumekuwa na malalamishi kutoka kwa wakazi wa kaunti ya Murang’a kuhusu huduma duni katika hospitali za umma akisema hatua aliyochukua huenda ikaleta mabadiliko.
Aliagiza pia kuwekwa kwenye mfumo wa dijitali mipango yote ya usimamizi wa hospitali na vituo vingine vya afya 157 vilivyo katika kaunti ya Murang’a ili kuboresha utoaji huduma.
Kuhusu ukosefu wa dawa, hata baada ya serikali ya kaunti kuhakikisha uwepo wake, gavana Irungu alisema kuna uwezekano kwamba dawa zinazotolewa na serikali huibwa kutoka hospitalini.
Wasimamizi wa sekta ya afya katika kaunti ya Murang’a wamepatiwa muda wa mwezi mmoja kuweka mfumo wa kidijitali la sivyo wachukuliwe hatua.
Hata hivyo, Irungu anatambua kwamba kumekuwa na vuzuizi kadhaa katika kuweka mfumo dijitali na anaomba wananchi wawe wavumilivu.
Anataka mfumo huo uwekwe ili kukabili malalamiko kadhaa na kumwezesha kufuatilia usambazaji wa dawa na vifaa vya matibabu.