Timu ya taifa ya wanawake ya Nigeria almaarufu Super Falcons imelazimisha sare kappa dhidi ya mabingwa wa Olimpiki Canada katika mchuano wa ufunguzi wa kundi B mapema Ijumaa mjini Melbourne nchini Australia.
Nigeria walidumisha rekodi ya kutoshindwa na Canada huku wakidhihirisha mchezo wa hali ya juu.
Canada walikosa fursa ya kufunga bao kupitia penalti ya mwanzoni mwa kipindi cha pili kipa wa Super Falcons Chiamaka Nnadozie akipangua tobwe la Christine Sinclair.
Nigeria walisalia wachezaji 10 uwanjani kunako dakika za mwisho mwisho baada ya Deborah Obiadun kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya VAR kubadilisha kadi ya awali ya njano.
Matokeo hayo yanawaweka wenyeji Australia uongozini kwa alama 3, wakifuatwa na Canada na Nigeria kwa alama moja kila moja.
Fainali za Kombe la Dunia zinaandaliwa kwa pamoja na Newzealand na Australia.