Viongozi wahimiza utulivu Isiolo

Walizungumza katika mazishi ya watu sita waliouawa kwenye shambulio la hivi karibuni la majambazi wadi ya Burat, kaunti ya Isiolo.

Marion Bosire
2 Min Read
James Lowasa, Naibu Gavana, Kaunti ya Isiolo

Viongozi wa kaunti ya Isiolo wametoa wito wa utulivu na amani kufuatia mazishi ya watu sita waliouawa katika shambulio la hivi karibuni la majambazi wadi ya Burat, kaunti ya Isiolo.

Waathiriwa wa jamii ya Turkana, walizikwa huku hasira zikiongezeka miongoni mwa wanajamii na viongozi wakionya dhidi ya mashambulizi ya kulipiza kisasi yanayoweza kusababisha umwagikaji zaidi wa damu.

Naibu Gavana James Lowasa aliwataka wakazi kujizuia na kudumisha utulivu, akisema kulipiza kisasi kutazidisha ukosefu wa usalama na kudhoofisha maendeleo.

Pia aliwataka viongozi wa kisiasa kuungana kutafuta suluhu ya changamoto za kiusalama zinazohusishwa na kaunti jirani za Garissa, Wajir, Samburu na Marsabit.

Lowasa alitaja ukame wa muda mrefu na ushindani wa maji na malisho ya mifugo kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea migogoro kati ya jamii za wafugaji.

Mwakilishi wa wadi ya Burat, Nicholas Lorot na mkazi Agostino Ekitella walihusisha mapigano ya mara kwa mara na mizozo ya mipaka ambayo haijatatuliwa kati ya Oldonyiro na Burat.

Seneta wa Isiolo, Fatuma Dullo, alilaani mauaji ya watu sita katika shambulio moja akielezea wasiwasi kuhusu madai ya uvamizi wa ardhi ya Isiolo kutoka kaunti ya Garissa.

Kamishna wa Isiolo, Chaunga Mwachaunga, aliahidi kupanga mkutano wa wadau kujadili hali ya usalama na mizozo ya mipaka.

Viongozi hao wametaka serikali kuchukua hatua za pamoja na kuimarisha mazungumzo ili kuzuia mauaji zaidi na kurejesha amani ya kudumu.

Share This Article