Pokot Magharibi mabingwa wa soka ya wanaume KICOSCA 2026

Hii ni baada ya kuilaza Nairobi mabao 5-3 kupitia penalti katika fainali iliyochezwa uwanjani Makutano, Kapenguria.

Marion Bosire
1 Min Read

Kaunti ya Pokot Magharibi imetwaa ubingwa wa soka ya wanaume katika awamu ya 13 ya mashindano kati ya serikali za kaunti almaarufu KICOSCA mwaka 2026.

Hii ni baada ya kuilaza Nairobi mabao 5-3 kupitia penalti katika fainali iliyochezwa Uwanjani Makutano, Kapenguria.

Timu hizo zilitoka sare tasa katika dakika 90 za kawaida na muda wa nyongeza, kabla ya Pokot Magharibi kuonyesha umahiri katika penalti na kutwaa ubingwa wake wa nne wa soka katika mashindano hayo.

Ushindi huo pia uliiwezesha Pokot Magharibi kumaliza mashindano bila kupoteza mchezo wowote, huku maelfu ya mashabiki wa nyumbani wakishangilia kwa furaha baada ya timu yao kutwaa taji hilo mbele yao.

Pokot Magharibi ilifuzu kwa fainali baada ya kuichapa Kakamega mabao 2-0 katika hatua ya nusu fainali.

Gavana wa Pokot Magharibi, Simon Kachapin alisifu mashindano hayo kwa kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa jamii.

Kachapin alisema kuandaa mashindano hayo ni tukio la kukumbukwa kwa kaunti yake, akibainisha kuwa yaliwakutanisha washiriki kutoka kaunti mbalimbali, tamaduni tofauti na vipaji vya michezo huku yakikuza urafiki na umoja kupitia ushindani wa kimichezo.

Share This Article