Timu ya taifa ya Kenya kwa vipusa, Harambee Starlets, imefuzu kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika (WAFCON) mwaka ujao baada ya kuizabua Gambia bao moja kwa bila katika mkumbo wa pili wa raundi ya pili uliosakatwa Jumanne jioni nchini Senegal.
Goli pekee la ushindi kwa Kenya lilifungwa na Mwanahalima Adam kunako kipindi cha pili.
Kenya iliyokuwa imeshinda duru ya kwanza mabao 3-1 wiki jana uwanjani Nyayo imefuatiliza kwa ushindi mwingine na kusajili ushindi wa jumla wa mabao 4-1.
Starlets wanaonolewa na Beldine Odemba wamefuzu kucheza WAFCON mwezi Machi mwaka ujao nchini Morocco kwa mara ya pili tangu mwaka 2016.