Serikali imekusanya bunduki haramu zaidi ya 600 katika bonde la Kerio katika juhudi za kudhibiti ukosefu wa usalama katika eneo hilo, haya ni kulingana na Rais William Ruto.
Rais amewataka wale ambao bado wanamiliki silaha haramu kuzisalimisha kwa hiari kwa vyombo vya usalama au wakabiliwe vikali kisheria.
“Tunawajua wote wenye bunduki na tutakuja kuzichukua” alisema Rais alipohutubia wakazi wa mji wa Kabarnet, Kaunti ya Baringo, leo Jumanne.
Aliongeza kusema kuwa eneo hilo haliwezi kuendelea kuwa la wajane na mayatima na hivyo akaelekeza waziri wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen, kuhakikisha kuwa bunduki zote zinakuwa mikononi mwa maafisa wa usalama.
Rais alisema serikali imejizatiti kumaliza ukosefu wa usalama hali iliyodumu zaidi ya miongo mitatu katika eneo hilo,na ambayo imesababisha vifo na uharibifu wa mali.
Rais Ruto alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika maeneo ya Marigat na Kabarnet, Kaunti ya Baringo, leo Jumanne.
Waliokuwa wameandamana na Rais kwa ziara hiyo Gavana Benjamin Cheboi, Mawaziri Murkomen wa usalama wa ndani na Hannah Cheptumo wa Jinsia na Utamaduni.
Wengine ni wabunge, wawakilishi wadi na viongozi wengine.
Waziri Murkomen alisema kati ya bunduki 602 haramu zilitwaliwa na vyombo vya usalama katika Bonde la Kerio, 120 zilitoka Kaunti ya Baringo.
Aliahidi kutokubali kurudi nyuma katika oparesheni ya kukabiliana na watu wanaomiliki silaha haramu.
