Jamii ya Ameru, Isiolo yatoa wito wa joto la kisiasa kutulizwa

Bruno Mutunga
2 Min Read

Viongozi wa jamii ya Ameru katika kaunti ya Isiolo, wakijumuisha koo zote nne za Igembe, Tigania, Imenti na Tharaka Nithi, wametoa wito wa kutuliza hali ya kisiasa ambayo wameielezea kuwa hasi, na kuwataka wakazi wote wa Isiolo kuipa serikali ya kaunti iliyo madarakani muda wa kufanya kazi kwao katika kipindi kilichosalia cha miaka miwili ya muhula wao.

Walisema kuwa watu wa Isiolo tayari wamepoteza mwaka mmoja kutokana na mchakato wa kisiasa wa kujaribu kumwondoa Gavana Abdi Guyo afisini, na hawawezi kuendelea kupoteza muda zaidi.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke wa Kaunti ya Isiolo, Geoffrey Kinyua Nabea, pamoja na walezi na wenyeviti wa koo hizo nne, walibainisha kuwa jamii ya Ameru, ambayo ni miongoni mwa jamii zenye idadi kubwa zaidi katika kaunti hiyo, inaendelea kuunga mkono serikali iliyo madarakani, iwe ya kitaifa ama ya kaunti.

Kinyua aliwahimiza wale ambao bado hawajakubali kwamba Gavana Abdi Guyo amenusurika kuondolewa madarakani kupitia hoja ya kumtimua, watambue kwamba kuna miaka miwili pekee kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Aliwasihi waipe serikali iliyoko madarakani nafasi ya kutoa huduma bila kuanzisha hali ya kisiasa isiyo na umuhimu wowote mapema.

Viongozi wa jamii hiyo waliisifu hatua ya Gavana Guyo ya kuwafikia wapinzani wake wa kisiasa kwa nia ya kuweka maridhiano baada ya kunusurika kuondolewa mamlakani, akifanikiwa kuwashawishi angalau madiwani 12 kati ya 18 waliokuwa wakiunga mkono hoja ya kuondolewa kwake madarakani ili wafanye kazi naye kwa muda uliosalia.

Pia waliwataka wakaazi wote wa Isiolo kutambua juhudi za gavana kuhakikisha mazingira ya amani baada ya siutofahamu za kisiasa zilizotokana na hoja ya kumng’oa madarakani, na kusubiri msimu wa siasa ili kutoa maoni yao badala ya kuanza kampeni mapema.

Hellen Makena, mkazi wa wadi ya Wabera, na Lydia Ntinyari kutoka wadi ya Bulapesa, walitambua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa katika wadi zao kupitia serikali ya Gavana Guyo, wakionyesha matumaini kwamba miradi zaidi itatekelezwa kabla ya kuanza kwa kampeni za kisiasa zijazo.

Bruno Mutunga
+ posts
Share This Article