Usimamizi wa hospitali ya kaunti ya Longisa katika kaunti ya Bomet umefanyiwa mabadiliko kufuatia kifo cha msichana mwenye umri wa miaka 3, Ruth Chepngeno, aliyefariki baada ya kuumwa na nyuki. Msichana huyo alidaiwa kufariki kutokana na utepetevu wa maafisa wa utabibu.
Kamati ya Afya ya Bunge la Bomet, ikiongozwa na mwenyekiti wake Stephen Changmorik imekiri kuwepo mapungufu wakati wa uhamishiaji mtoto huyo kwenye hospitali ya kibinafsi.
Chepngeno alibainika kufariki punde baada ya kufikishwa katika hospitali ya Tenwek baada ya kudaiwa kusubiri kwa zaidi ya saa tano bila kutibiwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Longisa.
Chepngeno alikuwa miongoni mwa watoto wanne walioshambuliwa na nyuki katika kijiji cha Koitabai, wadi ya Kembu katika eneo bunge la Bomet Mashariki.
Kufuatia kifo hicho na malalamiko mengine mengi yaliyotolewa na wagonjwa, usimamizi wa hospitali ya Longisa sasa umefanyiwa mabadiliko.
Mabadiliko hayo yanajumuisha uteuzi wa Dkt. Ronald Kibet kuwa msimamizi mkuu wa hospitali hiyo akichukua mahali pa Dkt. Andrew Cheruiyot, ambaye sasa atasimamia kliniki maalum.
Dkt. Benard Sowek, ambaye awali alihudumu kama Afisa Mkuu wa Afya na Ufuatiliaji ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Afya wa kaunti hiyo.