Rais William Ruto amempongeza Papa Mpya Leo XIV, baada ya kuchaguliwa leo Alhamisi kuliongoza Kanisa Katoliki.
“Hongera Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuchaguliwa kuwa Papa Mtakatifu wa 267 wa Kanisa Katoliki. Uongozi wako uwe wenye upendo, matumaini, utakaokuwa na sauti kwa wasio na sauti, utakaoleta amani na kuponya migawanyiko kote duniani,” alisema Rais Ruto kupitia ukurasa wake wa X.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula alipongeza Leo XIV huku akimtakia mema anapoongoza Kanisa Katoliki.
“Uongozi wako uwe wenye Hekima, Amani na unaoongwa kwa mkono wa Mungu. Nakutakia afya njema na nguvu unapoongoza kanisa na kuleta matumaini kote duniani,” alisema Spika huyo kupitia ukurasa wa X.
Naye Spika wa bunge la Senate Amason Kingi , alisema anajiunga na waumini wa kanisa Katoliki kusherehekea kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV kuliongoza Kanisa Katoliki.
Spika huyo alimtakia Papa huyo mpya heri njema anapomrithi Papa Francis aliyefariki mwezi Aprili mwaka huu.
Papa Leo XIV alichaguliwa leo Alhamisi na Makadinali 133, na kuhitimisha mchakato uliokuwa umesubiriwa kwa hamu kuu ya kumchagua Papa Mya.