Kenya na UAE zatia saini mikataba 7 kuimarisha uhusiano

Tom Mathinji
2 Min Read
Kenya na UAE zatia saini mikataba 7 kuimarisha uhusiano.

Kenya na Muungano wa Mataifa ya Kiarabu (UAE), zimetia saini mikataba saba ya maelewano, inayolenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Hatua hii inajiri miezi kadhaa baada ya nchi hizo mbili kutia saini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi jijini Abu Dhabi, UAE, mwezi Januari.

Hafla ya kutia saini mikataba hiyo saba, ilishuhudiwa na Rais William Ruto na Naibu Waziri Mkuu na  aliyepia Waziri wa Mambo ya nje wa UAE  Sheikh Abdullah Bin Zayed Al Nahyan, katika Ikulu ya Nairobi.

Mikataba hiyo inajumuisha ushirikiano katika maswala ya Jeshi, Maendeleo ya Kiuchumi, Nishati, Uchukuzi, Forodha, kubuni baraza la pamoja la biashara na Maendeleo ya uchukuzi wa Reli.

Katika sekta ya Nishati, mkataba huo unalenga Nishati mbadala kwa lengo la kutekeleza utumizi wa nishati inayotokana na upepo, jua na mvuke, ubadilishanji teknolojia na utekelezaji kawi safi.

Kuhusu Uchukuzi, mkataba huo unakusudia kuimarisha ushirikiano katika reli, uchukuzi wa angani na barabarani, kuimarisha miradi ya pamoja, fursa za uwekezaji na kuboresha usalama wa miundo msingi na uvumbuzi.

Mkataba kuhusu forodha unalenga kuboresha utekelezwaji wa sheria, kukabiliana na biashara haramu, kuimarisha ubadilishanaji wa habari, kulainisha taratibu na kuimarisha udhibiti wa mipakani.

Ili kufanikisha ushirikiano wa sekta ya kibinafsi, nchi hizo mbili zitabuni baraza la pamoja la uhusiano wa karibu wa kibiashara, kuimarisha uhusiano wa uwekezaji na kutoa mapendekezo kwa serikali zote mbili.

Website |  + posts
Share This Article