Uongozi wa KBC waifariji familia ya Mambo Mbotela

Martin Mwanje
2 Min Read
Uongozi wa KBC ulipoitembelea familia ya marehemu Mambo Mbotela mtaani Langata
  1. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji nchini, KBC, Agnes Kalekye leo Jumanne aliwaongoza maafisa wa ngazi za juu wa shirika hilo katika kuitembelea na kuifariji familia ya mtangazaji wa zamani wa shirika hilo Leonard Mambo Mbotela. 

Mambo, aliyefahamika sana kutokana na kipindi chake cha ‘Je, Huu ni Uungwana?’ alifariki Ijumaa wiki iliyopita wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.

Alifariki akiwa na umri wa miaka 85.

Ujumbe wa KBC ulimjumuisha Mhariri Mkuu Samuel Maina, Meneja wa Redio Mary Daraja na Meneja wa Masoko Florence Migunde miongoni mwa maafisa wengine.

Uongozi wa KBC ulipoitembelea familia ya marehemu Mambo Mbotela mtaani Langata

Wote hao walikutana na mjane wa marehemu, wanawe na nduguye Mambo Mbotela nyumbani kwake mtaani Langata na kuwafariji kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Kalekye amemsifia Mbotela kwa kuwa kielelezo chema katika jamii akiongeza kuwa alikuwa mtangazaji mahiri ambaye jina lake daima litaandikwa katika nyoyo za wengi kwa wino usioweza kufutika.

Rais William Ruto, Naibu wake Prof. Kithure Kindiki, Mawaziri, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ni miongoni mwa waliomwomboleza mtangazaji huyo nguli aliyekuwa daima mchangamfu na mcheshi kwa waliomfahamu.

Mbotela hakuwa tu mtangazaji bali pia mwimbaji hodari aliyewatumbuiza wafuasi wake katika maeneo mbalimbali ya burudani.

 

Website |  + posts
Share This Article