Mchekeshaji kwa jina Baba Kaunty ambaye awali alifahamika kama Mama Kaunty, amesema kwamba ameodnoka kwenye kipindi cha mitandaoni cha Obina Show.
Baba Kaunty alichapisha video mitandaoni akielezea uamuzi wake wa kujiondoa kwenye kipindi hicho akisema haukuwa uamuzi rahisi.
Kwenye video hiyo, mchekeshaji huyo alisema alikuwa akiwaza kuhusu kuondoka kwa muda wa miezi kadhaa na akasisitiza kwamba hakushurutishwa na yeyote kuondoka.
Hata ingawa hakutaka kuzungumzia suala hilo hadharani, Baba Kaunty alisema alilazimika kupaaza sauti ili kuzuia minong’ono isiyo sahihi.
Migogoro kuhusu mipangilio katika kipindi cha Obina Live ni mojawapo ya sababu ambazo zilimfanya Baba Kaunty aondoke.
Anasema kipindi hicho hupeperushwa kila Jumatatu na kuna shughuli nyingine ambazo anapaswa kufanya Jumatatu kama vile mafunzo ambayo anasema yataendelea kwa miezi mitatu.
Jamaa huyo alimsifia Obina akimtaja kuwa mfano wa kuigwa na ndugu ambaye alimpa fursa ya kujifunza mengi akiongeza kwamba Obina pekee ndiye anaelewa maono yake.
Baba Kaunty sasa ataangazia uundaji wa maudhui ya mitandaoni pamoja na watoto wa mtaa wa mabanda wa Kibera kupitia kwa wakfu wake uitwao Baba Kaunty Initiative.
Nafasi yake katika kipindi cha Obina imechukuliwa na binti kwa jina Pamela ambapo Baba Kaunty anasema yeye ndiye alimpendekeza na kuwasiliana naye ili achukue nafasi hiyo.
Baba Kaunty ndiye wa pili kuondoka kwenye Obina Live Show baada ya Dem wa Facebook ambaye aliamua kutozungumzia suala hilo.