Wizara ya Fedha ya Uganda imetangaza mpango wa kukopa dola milioni 150 kutoka kwa benki ya Exim ya China ili kuendeleza miundombinu ya intaneti nchini humo.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia wa Uganda na naibu waziri wa fedha aliwasilisha pendekezo hilo siku ya Jumatatu kwa kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya uchumi wa taifa.
Hatua hiyo inaangazia jinsi Uganda inavyozidi kutegemea ufadhili wa China baada ya Benki ya Dunia, mojawapo ya wafadhili wake wakuu, kusitisha ufadhili wake mwezi Agosti kutokana na hatua ya nchi hiyo kupitisha sheria tata ya kupinga mapenzi ya jinsia moja.
Uganda hapo awali ilichukua mkopo wenye utata wa dola milioni 200 kutoka kwa benki ya China ili kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe.
Mkopo huo umekosolewa na baadhi ya watu kuwa unaweka masharti ya kinyonyaji kwa Uganda.
Uganda pia iko katika mazungumzo na wakala wa mikopo wa nje wa China Sinosure kwa mkopo wa kusaidia kufadhili bomba la $5bn ambalo Uganda inapanga kutumia kusafirisha mafuta ghafi nchini Tanzania.