Uchaguzi wa AUC: Mawaziri wa Mambo ya Nje waanza kikao Ethiopia

Martin Mwanje
2 Min Read

Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wameanza kikao kisichokuwa cha kawaida kinachofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, AU mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Kikao hicho kitazingatia ripoti ya maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wakuu wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC kabla ya uchaguzi wa viongozi hao uliopangwa kufanywa mwezi Februari mwakani.

Viongozi wakuu wa AUC huchaguliwa kuhudumu kwa kipindi cha miaka minne, huku wakiwa na fursa ya kuchaguliwa kuhudumu kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Nyadhifa zinazoshindaniwa ni zile za mwenyekiti wa AUC, Naibu wake na makamishna sita wa tume hiyo.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza nia yake ya kuwa mwenyekiti mpya wa AUC.

Wadhifa huo kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki Mahamat kutoka Chad ambaye muda wake wa kuhudumu utamalizika mapema mwaka 2025.

Serikali ya Kenya ikiongozwa na Rais William Ruto imekuwa ikifanya kampeni ya kumtafutia Raila uungwaji mkono ili amrithi Mahamat.

Marais Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda na Samia Suluhu wa Tanzania ni miongoni mwa viongozi wanaosemekana kumuunga mkono Raila kutwaa wadhifa huo.

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo pia anampigia Raila upato wa kuwa mwenyekiti mpya wa AUC.

Hadi kufikia sasa, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Somalia Fawzia Yusuf Adam ametangaza nia ya kuwania wadhifa huo.

 

 

Share This Article