TSC yatangaza nafasi elfu 20 za walimu wanagenzi

Marion Bosire
1 Min Read

Tume ya Kuajiri Walimu Nchini, TSC imetangaza nafasi elfu 20 za walimu wanagenzi katika shule za umma za msingi na sekondari ya chini, JSS. 

Kulingana na tangazo la tume hiyo, nafasi elfu 18,000 ni za walimu wa JSS na elfu 2 ni za walimu wa shule za msingi.

Mpango huo wa uanagenzi wa walimu utakuwa wa kipindi cha mwaka mmoja na nia yake ni kuwapa ujuzi wanaojiunga na taaluma ya ualimu nchini.

Baada ya mwaka huo mmoja, kila mmoja atapokea cheti.

Walimu wanagenzi wa shule za msingi watakuwa wanalipwa elfu 15 kwa mwezi na wa JSS watapokea malipo ya elfu 20 kila mwezi.

Makataa ya kutuma maombi ya nafasi hizo ni Julai 10, 2023.

Ili kuhitimu kupata nafasi hizo, walimu wanagenzi wanaolenga kufunza katika shule za JSS watahitajika kuwa raia wa Kenya waliosajiliwa na TSC.

Pia watahitajika kuwa wamehitimu masomo ya ualimu kwa stashahada, gredi ya shule ya upili iwe C+ na wawe walipata kwenye KCSE alama ya C+ katika masomo mawili ambayo watafunza.

Wanaotaka kufunza katika shule za msingi wanahitajika kuwa na cheti cha P1, wawe raia wa Kenya na wamesajiliwa na TSC.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *