Ni afueni kwa timu ya taifa ya soka ya Iran baada ya wachezaji wake kupata viza za kuingia Marekani, na kuwapa matumaini ya kushiriki kinyang’anyiro cha kuwania Kombe la Dunia juma lijalo.
Viza hizo zimetolewa siku 10 tu kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya New Zealand, inayotarajiwa kuchezwa Los Angeles tarehe 15 mwezi Juni.
Kulingana na taarifa kutoka Marekani, viza hizo zimetolewa kwa wachezaji na wasaidizi hao, huku Tehran ikiishtumu Marekani kwa kuwanyima viza baadhi ya maafisa muhimu wa timu hiyo.
Aidha Marekani iliongeza kuwa haitaruhusu timu ya Iran kutumia mfumo huo kuingiza magaidi nchini Marekani.
Mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yanatarajiwa kuanza tarehe 11 mwezi Juni, wenyeji wa mechi hizo wakiwa Marekani, Canada na Mexico.