Taifa la Tanzania linaonekana kupiga hatua katika azimio lake la kuhakikisha matumizi ya kawi safi kama mojawapo ya njia za kulinda mazingira.
Hii ni baada ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, kukariri agizo la kutaka sehemu za umma zinazohudumia watu zaidi ya 100 kukoma kutumia makaa na kuni katika kuandaa chakula.
Majaliwa aliyezungumza jana kwenye tamasha la Kizimkazi katika mkoa wa Lindi, alisema kwamba siku ya mwisho ya kutumia mkaa na kuni kwa taasisi hiyo ilikuwa jana Disemba 31, 2024.
Maeneo yanayolengwa katika agizo hilo ni pamoja na taasisi kama Majeshi mbalimbali, Shule za bweni za binafsi na za Serikali, Magereza pamoja na Wazabuni wanaopika vyakula vya zaidi ya Watu 100.
Tanzania inaazimia kuhakikisha kwamba kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya raia wake wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuepuka athari za kiafya na uharibifu wa mazingira.
Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote nchini Tanzania kuhakikisha ajenda ya matumizi ya nishati safi inaangaziwa kwenye mikutano na shughuli zao mbalimbali.
Viongozi hao wanatarajiwa kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kuhusu uzuri wa kutumia nishati safi na athari za matumizi ya nishati ya kupikia inayoathiri mazingira.
Waziri Mkuu alitaja magonjwa mbali mbali kama vile ya macho, pumu, ya mapafu, maumivu ya kifua na magonjwa ya moyo kama miongoni mwa athari zinazowakumba kina mama na wasichana wengi kutokana na kutumia kuni na mkaa kupika.