Tanzania: Rais Samia awafukuza kazi Nape na Makamba

Martin Mwanje
3 Min Read

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaondoa katika nafasi za uwaziri, mawaziri wake wawili waandamizi. 

Wao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye. Pia amemuondoa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato.

Nape na Byabato wameondolewa ikiwa ni chini ya wiki moja tangu Nape anukuliwe akisema angemsaidia Byabato ambaye ni mbunge wa Bukoba Mjini, kaskazini magharibi mwa Tanzania kushinda ubunge katika uchaguzi wa 2025 kwa sababu anafahamu mbinu za uchaguzi na kwamba matokeo ya uchaguzi hayategemei ‘box’ (sanduku la kura) bali yanategemea nani anasimamamia uchaguzi na kuhesabu kura.

Kauli hiyo ilikosolewa na kupingwa katika majukwaa mbalimbali yakiwemo ya mitandao ya kijamii kwa tuhuma za kukiuka misingi ya demokrasia ya uchaguzi na kuheshimu uamuzi wa wapiga kura. Hata hivyo, Nape aliomba radhi kwa kauli yake hiyo huku akisema huo ulikuwa ni utani uliodumu kwa miaka tisa tangu atoe kauli nyingine tata kwamba chama tawala CCM kingeshinda uchaguzi wa 2015 hata kupitia bao la mkono.

Nafasi ya Nape inachukuliwa na Jerry Slaa aliyehamishwa kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, wakati nafasi ya Byabato itakaliwa na mbunge wa Mikumi Dennis Londo.

Pia kuan Naibu Waziri mpya mwingine wa Mambo ya Nje, mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi, anayechukua nafasi ya balozi Mbarouk Nassor Mabarouk aliyetangaza mapema Jumapili kujiuzulu lakini taarifa ya Ikulu imesema atapangwa kituo cha kazi.

TH

CHANZO CHA PICHA,FOREIGN.GO.TZ

Maelezo ya picha,Bado hakuna sababu za dhahiri za kuondolewa kwa Waziri wa Mambo ya Nje

Bado hakuna sababu za dhahiri za kuondolewa kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Makamba ambaye amewahi pia kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira, pia Waziri wa Nishati. Nafasi ya Makamba sasa inachukuliwa na Mahmoud Thabiti Kombo aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia.

Katika mabadiliko hayo, Waziri mpya wa Ardhi na Makazi ni Deogratius Ndejembi ambaye awali alikuwa Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu.

Aliyekuwa naibu waziri wa menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete sasa anakuwa waziri kamili wa Kazi. Ridhiwani ni mtoto wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Nafasi ya naibu waziri iliyoachwa wazi na Ridhiwani inajazwa na Deus Clement Sangu.

Kadhalika kuna uuteuzi na mabadiliko ya nafasi nyingine kwa adhi ya makatibu wakuu, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na taasisi za umma.

Kwa mara nyingine, Rais Samia amewaondoa maafisa waandamzi kadhaa katika ofisi ya rais Ikulu na kuwapangia majukumu mengine.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *