Kujifungua ni mojawapo ya nyakati muhimu katika maisha ya mwanamke, na huambatana na furaha ya kumkaribisha mtoto mchanga. Hata hivyo, kwa baadhi ya wanawake, muda mfupi baada ya kujifungua hugeuka kuwa mapambano ya kuokoa maisha yao kutokana na kuvuja damu nyingi.
Hali hiyo inayojulikana kitaalamu kama Postpartum Haemorrhage (PPH), ni mojawapo ya sababu kuu za vifo vya kina mama duniani. Katika Kaunti ya Tana River, changamoto za upatikanaji wa huduma za dharura za afya ya uzazi zinaendelea kuongeza hatari kwa wanawake wanaokumbwa na tatizo hilo.
Kwa Hadija Hussein, siku iliyoanza kama kawaida iligeuka kuwa tukio la kutisha baada ya kuanza kuvuja damu ghafla akiwa nyumbani.
Katika mahojiano ya moja kwa moja na Hadija, anasema alikuwa amehudhuria kliniki za wajawazito na kufanyiwa vipimo vilivyohitajika, lakini hali yake ilibadilika ghafla siku moja alipokuwa akiendelea na shughuli zake za kila siku.
Akiwa na ujauzito wa miezi minane, anasema alianza kuumwa na kuvuja damu asubuhi. Alikimbizwa katika Hospitali ya Bura kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Kaunti ya Rufaa ya Hola, alikofanyiwa upasuaji.
“Nikiwa na ujauzito wa miezi minane wa mtoto wangu wa tano, niliamka asubuhi na kuwapeleka watoto shule. Baadaye, nilianza kuumwa na kuvuja damu ghafla. Nilikuwa pia na tatizo la shinikizo la damu ambalo niliambiwa lilichangia hali yangu. Damu iliendelea kuvuja kuanzia asubuhi hadi saa saba mchana.
“Nilipoletwa katika Hospitali ya Hola, nilifanyiwa uchunguzi na kuambiwa mtoto hakuwa katika hali nzuri tumboni. Nilipelekwa kufanyiwa upasuaji. Watoto hao wengine sikupata changamoto kama hii. Kwa sasa namshukuru Mungu niko salama, na mtoto pia yuko salama,” anasema Hadija.

Kwa Husna, hali ilikuwa ya kutisha vilevile. Anasema alianza kuumwa na kichwa kabla maumivu kuongezeka akiwa hospitalini, hali iliyosababisha kuhitaji huduma maalumu katika Hospitali ya Rufaa ya Hola, kaunti ya Tana River.
“Nilianza kuumwa na kichwa na kwenda hospitalini. Maumivu yalizidi nikiwa huko. Kuanzia saa kumi jioni hadi saa sita usiku ndipo nilipofanyiwa upasuaji hapa Hola. Nilitoka Hospitali ya Bura, Tana River, baada ya kubainika kuwa kiwango cha damu mwilini mwangu kilikuwa chini,” anasema Husna.
Visa vya Hadija na Husna vinaangazia hatari zinazowakabili wanawake wakati wa kujifungua, hasa katika maeneo ambako huduma maalumu za dharura hazipatikani kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uchambuzi wa Masuala ya Kijinsia ya Sensa ya Kitaifa ya Idadi ya Watu na Makazi ya Kenya ya mwaka 2019, iliyoandaliwa na Shirika la Kitaifa la Takwimu nchini Kenya (KNBS), Kaunti ya Tana River ilirekodi kiwango cha vifo vya kina mama cha 586 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa wakiwa hai, na kuifanya kuwa miongoni mwa kaunti zilizokuwa na mzigo mkubwa wa vifo vya kina mama humu nchini.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Hola, wahudumu wa afya wanasema wamekuwa wakishuhudia madhara makubwa yanayotokana na kuvuja damu nyingi baada ya akina mama kujifungua.
Margaret Kariuki, msimamizi wa wodi ya wazazi katika hospitali hiyo, anasema baadhi ya wanawake waliopata tatizo hilo wamekumbwa na matatizo makubwa ya kiafya, yakiwemo figo kushindwa kufanya kazi.

Anasema kuvuja damu kupita kiasi kunaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, yakiwemo mfuko wa uzazi kushindwa kujikaza baada ya kujifungua, majeraha wakati wa kujifungua na matatizo yanayoathiri uwezo wa damu kuganda.
“Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, tumekuwa na wakati mgumu kutokana na baadhi ya wanawake kupoteza damu nyingi kiasi cha figo zao kushindwa kufanya kazi. Baadhi yao hulazimika kufanyiwa matibabu ya kusafishwa damu (dialysis), jambo ambalo pia huongeza mzigo wa kifedha kwa familia zao,” anasema Kariuki.
Daktari wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dkt. Bruce Semo, anasema kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua kunaweza kumpata mwanamke yeyote, hata kama ujauzito wake ulikuwa wa kawaida na hakuwa na matatizo katika ujauzito au uzazi wa awali.
Anatahadharisha kuwa kuchelewa kupata matibabu ya dharura kunaweza kusababisha mshtuko wa mwili kutokana na upotevu mkubwa wa damu, kuharibika kwa viungo muhimu na hata kifo.
“Tatizo hili linaweza kutokea ghafla hata kwa mwanamke aliyekuwa na ujauzito wa kawaida kabisa. Ndiyo maana kila mwanamke anapaswa kujifungulia katika kituo chenye uwezo wa kutambua na kushughulikia matatizo yanayoweza kutokea kwa haraka,” anasema Dkt. Semo.
Anaongeza kuwa baadhi ya wanawake huhitaji kuongezewa damu, kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi au kufanyiwa upasuaji wa dharura ili kudhibiti damu inayovuja. Katika hali mbaya zaidi, kuondoa mfuko wa uzazi kunaweza kuwa hatua ya mwisho ya kuokoa maisha ya mama.
Licha ya hatari hiyo, wataalamu wanasema huduma za kliniki za wajawazito zina umuhimu mkubwa katika kutambua mapema matatizo yanayoweza kuathiri afya ya mama na mtoto, pamoja na kuandaa hatua za kukabiliana na dharura wakati wa kujifungua.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza mwaka 2016 kuongeza idadi ya mahudhurio ya kliniki za wajawazito kutoka mara nne hadi mara nane katika kipindi cha ujauzito, kwa lengo la kuboresha utambuzi na udhibiti wa matatizo yanayohusiana na ujauzito na kuimarisha afya ya mama na mtoto.
Hata hivyo, Kariuki anasema bado kuna changamoto ya wanawake kuhudhuria kliniki hizo mara kwa mara katika Kaunti ya Tana River.
Anasema umbali kutoka makazi ya wananchi hadi vituo vya afya, pamoja na maisha ya jamii zinazohamahama, hasa wafugaji, ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya wanawake kutokamilisha mahudhurio yanayopendekezwa.
“Tunapochambua takwimu zetu, tunapata kuwa angalau asilimia 80 ya wanawake hufikia mahudhurio manne ya kliniki, lakini ni asilimia isiyozidi 60 inayofikia mahudhurio manane yanayopendekezwa. Wengine wanaachia njiani kutokana na umbali wa vituo vya afya, na baadhi yao huamua kujifungulia nyumbani,” anasema Kariuki.
Mbali na changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya, lishe ya wajawazito pia ni suala linalohitaji kupewa kipaumbele.
Katika baadhi ya jamii, upatikanaji mdogo wa vyakula vyenye virutubisho muhimu unaweza kuchangia upungufu wa madini ya chuma na kiwango cha chini cha hemoglobini katika damu. Hali hiyo inaweza kuongeza madhara yanayotokana na kupoteza damu wakati wa kujifungua.
Kariuki anasema wanawake wajawazito wanahitaji lishe yenye madini ya chuma ya kutosha, lakini maisha ya jamii za wafugaji na kuhama kutoka eneo moja hadi jingine yanaweza kuathiri upatikanaji wa huduma za lishe na uchunguzi wa afya.
“Katika kaunti za maeneo kame na nusu kame, wengi ni wafugaji. Baadhi ya wanawake huwa na kiwango cha chini cha hemoglobini ambacho hakikidhi mahitaji ya ujauzito. Pia, umbali wa vituo vya afya na kuhama kwa wafugaji kutoka eneo moja hadi jingine hufanya baadhi ya wanawake kukosa mwendelezo wa huduma za kliniki,” anasema.
Katika ngazi ya jamii, juhudi zinaendelea kuhusisha wanaume zaidi katika masuala ya afya ya uzazi.
Mohammed Keisane, mhudumu wa afya ya jamii katika eneo la Bura, anasema baadhi ya wanaume wameanza kuwaandamana na wenzi wao kwenda katika kliniki za wajawazito, ishara ya kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu wa afya ya mama na mtoto.
Hata hivyo, anasema uhaba wa wahudumu wa afya na kuchelewa kwao kufika kazini wakati mwingine huathiri utoaji wa huduma za dharura kwa wanawake wanaohitaji msaada wakati wa kujifungua.
“Wanaume wanaoandamana na wake zao hospitalini ni wale wanaoelewa umuhimu wa kliniki za mama na mtoto. Hata hivyo, kuna wakati mwanamke anafika hospitalini akihitaji msaada wa haraka, lakini anakosa huduma kwa sababu daktari anayepaswa kuwa kazini hajafika kwa wakati. Wakati mwingine hulazimika kusubiri hadi mhudumu mwingine afike,” anasema Keisane.
Kwa wanawake wanaonusurika kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua, madhara hayaishii pale damu inapodhibitiwa.
Dkt. Semo anasema baadhi yao huendelea kukumbwa na hofu ya kupata ujauzito mwingine, msongo wa mawazo, kiwewe cha kisaikolojia na hata mfadhaiko wa akili.
Anasisitiza kuwa pamoja na matibabu ya kimwili, wanawake hao wanahitaji pia msaada wa kisaikolojia ili kuwasaidia kurejea katika hali yao ya kawaida.
“Tunapaswa kuzingatia pia athari za kihisia ambazo mara nyingi hazipewi uzito unaostahili. Wanawake wanaonusurika tatizo hili wanaweza kukumbwa na kiwewe cha kisaikolojia, wasiwasi, hofu ya kujifungua tena na mfadhaiko. Baadhi yao huchukua miezi kadhaa kupona kihisia,” anasema Dkt. Semo.
Athari za matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua zinaweza pia kuwakumba watoto wachanga.

Esther Ndara, afisa wa kliniki anayebobea katika afya ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Hola, anasema baadhi ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wao au kufuatia matatizo ya kiafya ya mama huhitaji uangalizi maalumu.
Anasema watoto wanaozaliwa katika kipindi cha wiki 34 hadi 36 za ujauzito wanaweza kuwa hawajakomaa kikamilifu, hivyo kuhitaji uangalizi wa karibu, msaada wa lishe na kuongezewa oksijeni hadi hali zao zitengemae.
“Baadhi ya watoto wanaozaliwa katika umri huo wa ujauzito huwa hawajakomaa kikamilifu. Tunawalisha, kuwapa oksijeni na kufuatilia hali zao kwa karibu ili kuhakikisha wanakuwa imara,” anasema Ndara.
Wakati huohuo, wahudumu wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Hola wanasema wanaimarisha juhudi za kutambua mapema wanawake walio katika hatari ya kuvuja damu nyingi na kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati.
Kariuki anasema wahudumu wa afya ya jamii wanaendelea kujengewa uwezo wa kutambua dalili za hatari, ikiwemo kuvuja damu kusiko kwa kawaida, na kuhakikisha wanawake wanaohitaji matibabu ya dharura wanapelekwa hospitalini bila kuchelewa.
Anasema pia ni muhimu kutambua matatizo ya damu kuganda, kama vile ugonjwa wa Haemophilia, ambao unaweza kusababisha damu kuendelea kutoka baada ya kujifungua.
Anasisitiza umuhimu wa kuwapa wahudumu wa afya ya jamii mafunzo yatakayowawezesha kushuku uwepo wa tatizo hilo mapema na kuwaelekeza wagonjwa kufanyiwa vipimo vinavyohitajika.
Innocent Wale, muuguzi anayesimamia huduma za matatizo ya damu katika Hospitali ya Hola, anasema hospitali hiyo huandaa kampeni za uchangiaji damu kila mwezi ili kuhakikisha kuna akiba ya kutosha kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu, wakiwemo wanawake wanaopata tatizo la kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua.
Anasema baadhi ya wanawake wenye Haemophilia wanaweza kutokujua kuwa wana tatizo hilo hadi wanapopata changamoto ya kuvuja damu baada ya kujifungua.
“Tunao wanawake wenye Haemophilia ambao wana upungufu wa vipengele vinavyosaidia damu kuganda. Mwanamke mwenye tatizo hili anapojifungua, damu inaweza kuendelea kutoka hata baada ya kujifungua. Bila uchunguzi, inaweza kuwa vigumu kubaini chanzo. Ndiyo maana kila mwanamke anayepata tatizo la kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua anapaswa kufanyiwa vipimo ili kubaini iwapo chanzo ni Haemophilia au tatizo jingine,” anasema Wale.
Kwa wanawake kama Hadija na Husna, kunusurika baada ya kuvuja damu nyingi kumeambatana na changamoto za kupata huduma maalumu kwa wakati.
Visa vyao vinaonyesha umuhimu wa kuimarisha maandalizi ya dharura, kuhakikisha wanawake wanahudumiwa na wataalamu wenye ujuzi wakati wa kujifungua, kuboresha mifumo ya rufaa na kuzipa hospitali vifaa na rasilimali zinazohitajika.
Ingawa kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua kunaweza kutokea bila kutarajiwa, madhara yake yanaweza kupunguzwa kupitia utambuzi wa mapema na matibabu ya dharura.
Furaha ya kumkaribisha mtoto duniani haipaswi kuishia kuwa kumbukumbu ya huzuni kwa familia iliyompoteza mama. Kuimarisha huduma za afya ya uzazi ni hatua muhimu katika kuhakikisha kila mwanamke anapata nafasi salama ya kujifungua na kurejea nyumbani akiwa hai na mwenye afya.