Spika Wetang’ula azuru waathiriwa wa ajali Webuye

Wetang'ula amelalamikia ajali za barabarani zinazoendelea kusababisha vifo vya wengi akisisitiza kuwa kama nchi, suala hilo linapaswa kushughulikiwa haraka.

Marion Bosire
2 Min Read

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula leo Jumatano amezuru waathiriwa wa ajali ya barabarani iliyotokea jana katika eneo la Malaha kwenye barabara kuu ya kutoka Webuye kuelekea Kitale.

Wetang’ula aliyekuwa ameandamana na viongozi kadhaa wa eneo hilo, aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo katika hospitali ya kaunti ya Webuye.

Alishauriana pia na familia za walioaga dunia kwenye ajali hiyo na kuhudhuria mazishi ya mmoja wao.

Wetang’ula alitangaza kubuniwa kwa kamati itakayosimamia mazishi ya walioaga dunia ikiongozwa na mbunge wa eneo la Webuye Mashariki Martin Wanyonyi Pepela na mwakilishi wa kike wa kaunti ya Bungoma Catherine Wambilianga.

Aidha aliashiria kuwa ibada ya pamoja ya mazishi kwa ajili ya walioaga dunia itaandaliwa Jumatatu, Machi 16, 2026 mjini Webuye, ibada itakayotumiwa pia kuombea waliojeruhiwa.

Wakati huo huo, Wetang’ula pia amelalamikia ajali za barabarani ambazo zinaendelea kuchukua maisha ya wengi, akisisitiza kwamba kama nchi, suala hilo linapaswa kushughulikiwa haraka.

“Tunalaani kabisa dereva mtepetevu wa lori aliyesababisha ajali hiyo katika makutano ya Malaha, kaunti ndogo ya Webuye na kusababisha vifo vya watu 15,” alisema Wetangula katika taarifa.

Majeruhi wapatao 21 wanaendelea kupokea matibabu katika taasisi mbalimbali za afya za eneo hilo.

Spika Wetang’ula alisema mipango imefanywa ya kuhamisha wawili kati yao waliohitaji matibabu maalum.

Alihimiza Mamlaka ya Kudhibiti Usalama Barabarani, NTSA kuchukua hatua mara moja kuhakikisha madereva watepetevu wanaondolewa barabarani.

Mahakama nazo hazikusazwa huku Wetang’ula akizitaka kuchukulia kwa uzito kesi za utepetevu barabarani na wanaosababisha ajali wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Kadhalika amelitaka bunge kuunda sheria bora za sekta ya uchukuzi akisema Rais William Ruto ameahidi kusaidia familia za waathiriwa.

Share This Article