Siku ya Mashujaa: Maandalizi yapamba moto

Sherehe za Siku ya Mashujaa mwaka huu zitaandaliwa katika uwanja wa Ithookwe, kaunti ya Kitui Oktoba 20, 2025. Maudhui ya siku hiyo ni "Kubadilisha Maisha Kupitia Suluhu za Nishati Endelevu."

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri Salim Mvurya akiongoza timu ya ukaguzi katika uwanja wa Ithookwe, kaunti ya Kitui.

Waziri wa Michezo Salim Mvurya aliongoza viongozi wengine katika kukagua uwanja wa Ithookwe uliopo katika kaunti ya Kitui ambako zitaandaliwa sherehe za Siku ya Mashujaa mwaka huu.

Mvurya aliandamana na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo na Gavana wa Kitui Dkt. Julius Malombe miongoni mwa viongozi wengine wakuu serikalini.

Katika uwanja wa Ithookwe, pirikapirika za kuhakikisha uwanja huo uko tayari zimepamba moto huku upakaji rangi ukiendelea na miundombinu mingine muhimu kuwekwa.

Timu hiyo ya ukaguzi ikielezea imani kuwa maandalizi yatakamilika kwa wakati unaofaa kabla ya kuandaliwa kwa sherehe za Siku ya Mashujaa Oktoba 20, 2025.

Rais William Ruto ataliongoza taifa katika kuadhimisha siku hiyo katika uwanja huo ambako watu mbalimbali (Mashujaa) watatuzwa kwa kubobea katika fani zao.

Maudhui ya Siku ya Mashujaa mwaka huu ni “Kubadilisha Maisha Kupitia Suluhu za Nishati Endelevu.”

Serikali ya Kenya Kwanza inasema maudhui hayo yanaangazia kipaumbele kinachotolewa kwa nishati kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

 

Website |  + posts
Share This Article