Kamishna wa eneo la Pwani, Rhoda Onyancha, amesema biashara zimeimarika katika kaunti ya Kwale, sherehe za Mashujaa zinapoandaliwa katika kaunti hiyo.
Kulingana na Onyancha wakazi wa Kwale na viunga vyake, wamenakili biashara iliyoimarika kutokana na idadi kubwa ya wageni wanaohudhuria sherehe hizo.
“Watu wa Kwale na Pwani kwa jumla wamefurahia sherehe hizi kuandaliwa hapa Kwale, hasaa wanabiashara ambao wamepata wateja wengi wakati huu,” alisema Onyancha.
Akizungumza Leo Jumamosi na shirika la utangazaji hapa nchini KBC katika hoteli moja eneo la Diani kaunti ya Kwale, Onyancha alithibitisha kuwa maandalizi ya sherehe za mwaka huu za siku kuu ya Mashujaa yamekamilika.
Mkuu huyo wa eneo la Pwani, alitoa wito kwa wageni wanaozuru kaunti hiyo kutumia fursa zilizopo na kuwekeza katika kaunti hiyo
Sherehe za mwaka huu za Mashujaa zinaandaliwa katika kaunti ya Kwale, kauli mbili ikiwa ni “Nyumba za gharama nafuu”.
Onyancha alisema hali ya usalama imeimarishwa kabla ya sherehe hizo siku ya Jumapili.