Serikali yasema eneo palipomwagika sodium cyanide sasa ni salama

Martin Mwanje
3 Min Read

Serikali ya Kenya imetangaza kuwa eneo la Kambembe huko Rironi katika kaunti ya Kiambu palipomwagika kemikali ya sodium cyanide sasa ni salama. 

Hii ni baada ya eneo hilo kusafishwa na kemikali hiyo kuondolewa.

Hata hivyo, Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni anasema mitungi kadhaa ya kemikali hiyo yenye sumu kali bado haijulikani ilipo na inashukiwa kuchukuliwa na watu wanaoishi karibu na eneo hilo.

“Ingawa hakuna visa vya sumu vilivyoripotiwa, Wizara imeanzisha utoaji wa taarifa juu ya hatari ya kemikali hiyo na ushirikiano wa jamii kupitia makanisa, taasisi kuu za utoaji huduma za afya, wahudumu wa afya, maafisa wa serikali kuu na wale wa Nyumba Kumi,” amesema Muthoni katika taarifa leo Jumatatu.

“Juhudi hizi zinalenga kufuatilia na kupata kemikali zozote ambazo huenda zimechukuliwa kimakosa na watu katika jamii.”

Muthoni ameonya kuwa kemikali hiyo ina sumu kali na umezaji au unusaji wa hata kiwango kidogo cha sumu hiyo unaweza ukasababisha kifo.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo serikali ya Marekani imetahadharisha raia wake walioko nchini Kenya wasipitie kwenye barabara kuu nambari A104 katika eneo la Kambembe kufuatia kumwagika kwa kemikali hiyo.

Raia hao walishauriwa kutumia barabara mbadala ya Limuru na kutopitia barabara kuu ya Waiyaki na wafuatilie taarifa kufahamu iwapo eneo husika limesafishwa na ni salama.

Lori lililokuwa limebeba kemilaki hiyo ya sodium cyanide lilihusika kwenye ajali na kusababisha kumwagika kwa kemikali hiyo barabarani na wakazi wanasemekana kuiiba.

Kemikali hiyo ni mbaya sana kwa binadamu na hata mazingira na inatambulika kama vidonge vidogo vya rangi nyeupe.

Awali, Wizara ya Afya ilitoa tahadhari ikiwasihi wakazi kutopita karibu na eneo hilo kama njia ya kuhakikisha usalama wao.

Katibu wa Wizara ya Afya Mary Muthoni alisema kwamba kumeza au hata kunusa kemikali hiyo ni hatari sana kwani kunaweza kusababisha matatizo ya neva mwilini.

Kwa upande wake,Mmamlaka ya Mazingira nchini, NEMA imeonya wote walioiba mitungi ya kemikali hiyo baada ya kutokea kwa ajali hiyo ikisema wanafaa kuiwasilisha kwa vituo vya polisi vilivyo karibu nao.

Inaripotiwa kwamba mitungi kadhaa iliibwa na watu waliojitokeza baada ya lori lililokuwa limebeba kemikali hiyo kuhusika kwenye ajali na kuanguka juzi Jumamosi huko Rironi.

Taarifa zaidi imechangiwa na Marion Bosire

Website |  + posts
Share This Article