Waziri wa elimu Julius Migos Ogamba, amekariri kujitolea kwa serikali kuwekeza zaidi katika taasisi za kiufundi za TVET, akizitaja nguzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi.
Ogamba aliyezungumza wakati wa sherehe ya kwanza ya kufuzu kwa wanafunzi wa taasisi ya kiufundi ya Maasai Mara TVET siku ya Ijumaa, alitambua jukumu muhimu ambalo hutekelezwa na wahandisi mafundi wa mabomba ya maji na wataalam wa hoteli, ambao ujuzi wao ni muhimu kwa maendeleo ya taifa hili.
“Ujuzi ambao umepokea katika taasisi hii, unakupa fursa ya kufanikisha ajenda ya mageuzi ya kiuchumi kutoka chini almaarufu Bottom-Up Economic Transformation Agenda. Ajenda hii inahusu kubuni nafasi za ajira, ufufuzi wa viwanda na kuhakikisha kila mkenya ananufaika na ukuaji wa uchumi,” alisema Ogamba.
Aliwahimiza mahafali hao kuwa wabunifu zaidi na kujiajiri, huku akiwataka kutumia ujuzi wao kutekeleza maendeleo.
Wakati huo huo, waziri huyo alisema wizara yake imeanza kuwatuma wakufunzi 2,000 katika taasisi za TVET kote nchini, ili kukabiliana na upungufu wa wakufunzi ambao umeshuhudiwa katika taasisi hizo.
Kwa upande wake naibu Gavana wa Narok Tamalinye Koech, aliyemwakilisha Gavana wa kaunti hiyo, alitoa wito kwa jamii ya eneo hilo kutumia fursa iliyopo ya tasisi hizo kuwawezesha watoto wao kupata elimu ya juu.
Taasisi ya TVET ya Maasai Mara ina wanafunzi 2,000 walio darasani kwa sasa na wengine 1,000 ambao sasa ni wanagenzi.