Katika kukabiliana na wasiwasi wa hivi karibuni kuhusu ubora wa mafuta ya petroli nchini Kenya, shirika la ubora wa bidaa nchini KEBS na mamlaka ya kawi EPRA zimetoa tamko la pamoja.
Katika taarifa mashirika hayo mawili yanathibitisha usalama na ufanisi wa usambazaji wa mafuta nchini.
Mashirika yote mawili yamefafanua kuwa mafuta yote ya petroli yanayoingizwa nchini yanapitia vipimo na uthibitisho mkali ili kukidhi viwango vya Kenya.
Ripoti na video za hivi karibuni zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zilisababisha mashirika haya kufanya vipimo vya ziada kwa sampuli za mafuta kutoka vituo mbalimbali vya kuuza mafuta vikiwemo vile vilivyotajwa katika ripoti hizo.
Matokeo ya vipimo yalithibitisha kuwa mafuta katika vituo vyote yanakidhi viwango vinavyohitajika vya RON, kama ilivyobainishwa katika viwango vya Kenya.
Zaidi ya hayo, mashirika hayo yalithibitisha kuwa Super Petrol, inayouzwa kama mafuta ya kiwango cha juu, ilikidhi viwango vya juu vya RON kama inavyohitajika.
KEBS na EPRA zinahakikishia umma kwamba licha ya kuibuka kwa vifaa vinavyodai kupima ubora wa mafuta, matokeo sahihi yanaweza kupatikana tu kupitia vipimo vya maabara vinavyofuata viwango sahihi.
Walisisitiza pia kwamba watumiaji wanapaswa kuwa na imani katika ubora wa mafuta yanayopatikana katika soko la Kenya.
Mashirika hayo pia yamewataka watumiaji kuendelea kutumia mafuta bila wasiwasi, kwani matokeo yao yanaonyesha hayajapotoka kutoka kwa viwango vya ubora vilivyowekwa.