Kenya haijalegeza kasi ya ukarabati wa miundo mbinu kwa fainali za kuwania Kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi za nyumbani (CHAN) mwezi Agosti mwaka huu.
Haya yamesemwa leo na Katibu katika wizara ya michezo Mhandisi Peter Tum, alipofungua warsha ya kamati andalizi ya CHAN katika Mkahawa wa uwanja wa kimataifa wa Kasarani.
Kulingana na Tum awamu ya pili ya ukarabati inatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
Kipute cha CHAN kitaandaliwa kati ya Agosti mbili na 30 mwaka huu kwa pamoja na Kenya, Uganda, na Tanzania.
Kenya imejumuishwa kundi A katika fainali za mwaka huu pamoja na mabingwa mara mbili DR Congo na Morocco, Zambia na Angola.