Wizara ya usalama wa ndani imewahakikishia wakazi walioathkrika na mafuriko katika kaunti ya Tana River kwamba serikali imeanza mipango ya kuwatafutia makao mapya.
Akizungumza Garsen wakati apotembelea jamii za waathiriwa wa mafuriko ,katibu mkuu katika wizara ya usalama wa ndani Raymond Omolo ,amesema kuwa serikali itanunua ardhi kutoka kwa watu binafsi katika eneo hilo ili kuwajengea nyumba za kudumu wakazi walioathirika kwenye mafuriko hayo.
Katibu huyo aidha amesema kuwa barabara zote ambazo ziliharibiwa na mafuriko hasa ile ya Gamba-Lamu pamoja na zile zinazoelekea kwenye vijiji zitakakarabatiwa.
Wakati huo huo Omolo amewahakikishia wanafunzi wa zaidi ya shule 19 za upili ambazo pia ziliathirika kwa mafuriko kuwa watapata msaada wa chakula ili kuendelea na masomo.
Aidha amewataka wakazi kuchukua taadhari hasa wakati kunapotokea mafuriko katika eneo hilo.
Watu wapatao 38,000 wameathiriwa na mafuriko huku wanane wakiripotiwa kufariki.
Mafuriko hayo pia yaliharibu zaidi ya ekari elfu 13,000 za mimea huku mifugo zaidi ya 1100 wakiangamia.