Serikali kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo nchi nzima

Marion Bosire
1 Min Read

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema kuwa serikali inapanga kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kote nchini iliyozinduliwa na Rais William Ruto.

Mwaura aliyasema hayo katika kikao na wanahabari leo Alhamisi baada ya ripoti kadhaa kuonyesha miradi iliyokwama inayodaiwa kutokana na ufisadi.

Alisema maafisa kutoka Ofisi ya Rais watafanya ukaguzi wa kina wa miradi yote ya maendeleo kwenye maeneo yote ya taifa ili kubaini hali halisi.

“Serikali imefanikisha mengi, lakini mara nyingi kuna mkanganyiko unaozunguka juhudi zake. Ofisi yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, itatembelea maeneo yote nchini,” Mwaura alisema.

“Tutahakikisha kwamba kile kilicho kwenye karatasi, na kile tunachojadili hapa Nairobi, kinafanyika mashinani,” Mwaura alisema.

“Kuna madai kwamba ukweli wa kimsingi unatofautiana na simulizi rasmi, na lazima tushughulikie mtazamo huu.”

Matamshi ya Mwaura yanajiri baada ya wakili Kebaso Morara kujitokeza na kufichua miradi yaliyozinduliwa ambayo yamekwama na mengine kukosa kutekelezwa.

Morara ambaye amegeuka kuwa mwanaharakati amesikika akilaumu serika kwa kile anachokiita ni utumizi mmbaya wa pesa za umma.

Share This Article