Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amewahakikishia Wakenya kwamba serikali itatafuta mbinu nyingine za kufadhili ukarabati wa barabara bila kuongeza bei za mafuta.
Murkomen amesema hatua hiyo inafuatia wasiwasi ulioibuliwa na wananchi wakati wa zoezi la kukusanya maoni, wakihofia kuwa bei ya bidhaa za mafuta huenda zikaongezeka iwapo serikali itaongeza ada za ukarabati wa barabara.
Kupitia kwa taarifa, Murkomen amesema wizara yake itatafuta mbinu mbadala za kufadhili ujenzi wa barabara bila kuongeza bei za mafuta.
“Hatua itachukuliwa tu baada ya kubainisha kuwa mbinu za kukusanya mapato hazitasababisha kupanda kwa gharama ya maisha,” alisema Murkomen.
Waziri aliahidi kutathmini upya mapendekezo yote yaliyotolewa na umma kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Kulingana na waziri huyo, Kenya kwa sasa inakabiliwa na nakisi ya ukarabati wa barabara ya shilingi bilioni 78 kwa mwaka wa fedha wa 2024, huku kiwango hicho kikitarajiwa kupanda hadi shilingi bilioni 315 kufikia mwaka wa fedha wa 2028/2029.
Mnamo mwezi uliopita, Murkomen aliiarifu kamati ya bunge kuhusu fedha na mipango ya kitaifa kwamba ada hiyo iliongezwa mara ya mwisho mwaka 2016 na inafaa kupitiwa upya.