Seneta wa kaunti ya Tana River Danson Mungatana amewasilisha katika bunge la Seneti hoja ya kujadili mienendo ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Mungatana anasema kwa mujibu wa Kifungu 147 cha Katiba, Naibu wa Rais ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais na kufanya anayeshikilia wadhifa huo kuwa nembo ya umoja wa taifa.
Kulingana naye, Naibu wa Rais ana jukumu la nyakati zote kuheshimu, kudumisha na kulinda katiba, kuhamasisha umoja wa taifa na heshima kwa watu na jamii mbalimbali zinazoishi nchini, kitu ambacho Gachagua amekiuka.
“Kwa kuwa na mashaka kwamba Rigathi Gachagua, mara kadhaa tangu aliposhika hatamu kama Naibu wa Rais, ametoa matamshi, miongoni mwa mengine, kuhusiana na fursa za ajira kwa Wakenya katika utumishi wa umma, ugavi wa rasilimali kwa kaunti na kuwachochea baadhi ya Wakenya kutotii maagizo ya kisheria yanayotolewa na baadhi ya serikali za kaunti;
“Na kwa kuelezea zaidi mashaka kuwa matamshi hayo kwa umma yanayotolewa na Naibu Rais yamewatenga baadhi ya Wakenya; kusababisha na yanazidi kusababisha hofu miongoni mwa jamii mbalimbali nchini…Seneti kwa mujibu wa kanuni nambari 101(1) inaelezea kutoridhika na kusikitishwa kwake na mienendo ya Rigathi Gachagua kama Naibu Rais na inamkosoa,” inaelezea hoja ya kutokuwa na imani na Gachagua iliyowasilishwa na Mungatana.
Hata hivyo, Waziri wa Mazingira Aden Duale amekosoa hatua ya Mungatana akisema hoja kama hiyo inaweza tu kuwasilishwa katika bunge la Taifa na wala siyo Seneti kwa mujibu wa Kifungu cha 150 cha Katiba.
Hoja hiyo, kulingana na Duale, inapaswa kuungwa mkono na wabunge 117 na kisha 233 ili kufikia lengo la kumtimua Gachagua.
Akijitetea, Mungatana amejibu kwa kusema kile alichowasilisha katika bunge la Seneti ni hoja ya kutokuwa na imani na Gachagua wala si ya kumbandua madarakani.
Gachagua ameunyoshea utawala wa Rais Ruto kidole cha lawama kwa kuitendea visivyo ofisi yake na kuapa kupigania haki zake kama Naibu Rais.
Baadhi ya viongozi akiwemo Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli wamemkosoa Gachagua wakimtaka kumheshimu Rais.
Hata hivyo, wengine wametoa wito kwa Rais Ruto na Gachagua kushiriki meza ya mazungumzo na kusuluhisha tofauti kati yao kwa manufaa ya taifa.