Sauti Sol kutengana kwa muda

Marion Bosire
1 Min Read

Kundi la muziki la Sauti Sol limetangaza kwamba litasambaratika kwa muda.

Mwanachama wa kundi hilo Bien Barasa alielezea kwamba tamasha wanayoandaa ya Solfest Novemba 4 ambayo imepatiwa jina la “Last Dance” ndiyo yao ya mwisho kabla ya msambaratiko huo wa muda.

Aliyasema hayo katika kikao na wanahabari ambapo pia walitangaza ushirikiano wao na Coke Studio, ambapo alielezea pia kuhusu maandalizi yao kwa tamasha hiyo ya watu mashuhuri almaarufu “VIP show”

Kulingana naye, tiketi za tamasha hiyo ambazo za bei ya shilingi elfu 25 tayari zimenunuliwa zote jambo ambalo ni la kufana.

Kundi hilo limekuwa likijiandaa kwa muda wa miezi miwili sasa kwa tamasha hiyo.

“Kwa miaka yote ambayo tumekuwa pamoja kama kundi hatujawahi kujiandaa kwa tamasha kwa bidii kama tunavyojiandaa kwa hii” alisema Bien.

Kuhusu kusambaratika kwa muda alisema kwamba ni vizuri kwenda mapumziko akisema huenda mashabiki walidhania ni taarifa tu za uongo mitandaoni lakini sivyo.

Mwaka jana kundi hilo liliadhimisha miaka 17, lilianzishwa mwaka 2005 na wanachama walikuwa Bien-Aimé Baraza, Willis Chimano, Savara Mudigi na Polycarp Otieno ambaye hucheza gitaa.

kampuni ya Coca-Cola inashirikiana na kundi hilo kama mdhamini ambapo itatoa vinywaji na kuhakikisha mashabiki wanapata muziki mzuri.

Tamasha hiyo itaandaliwa katika uwanja wa Uhuru Gardens.

Share This Article