Takriban wafanyakazi 2,000 wa shirika la Posta nchini wameanza mgomo kote nchini siku ya Alhamisi kulalamikia kutolipwa mshahara wa miezi mitano.
Katika kaunti ya Nairobi, wafanyakazi hao walikongamana katika tawi City Square la Posta wakistahimili mvua na baridi, huku wakibeba mabango na kuimba nyimbo za kutaka kutendewa haki.
Baadhi tuliozungumza nao walisema hali imekuwa ngumu huku wengine wakilazimika kufanya vibarua ili kupata nauli ya kufika kazini na chakula.
Hata hivyo, wafanyakazi hao waliapa kuendelea na mgomo hadi watakapolipwa malimbikizi ya mshahara wa miezi mitano, na kukataa ofa iliyotolewa na wizara ya leba na kusainiwa na katibu mkuu wa chama cha wafanyikazi wa sekta ya mawasiliano nchini -COWU Benson Okwaro.
Wafanyakazi hao walikuwa wameombwa kusitisha mgomo na kurejea kazini, huku wakiahidiwa kulipwa mshahara wote wa miezi mitano ifikiapo mwisho wa mwezi Novemba mwaka huu.
Kando na mshahara ambao hawajalipwa tangu Julai mwaka huu, pia wafanyakazi hao wa Posta wanataka kuwasilishwa kwa matozo ya lazima na yale ya mikopo ambayo hayajatumwa kwa benki na mashirika husika kwa zaidi ya miaka miwili, licha ya wao kukatwa.
Wameapa kutorejea kazini hadi pale watakapolipwa malimbikizi yote.
COWU ilikuwa imetoa makataa ya wiki tatu kwa mwajiri wa wafanyakazi hao kulipa malimbikizi hayo ifikiapo Oktoba 31.
Hata hivyo, wasimamizi wa Posta wanasema hali imekuwa ngumu kutokana na kutolipwa kwa madeni yao ikiwemo vituo vya Huduma Centre na tume ya IEBC.