Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje Korir Sing’oei ametangaza leo Alhamisi kwamba utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa njia ya kunyongwa kwa Mkenya Stephen Munyakho nchini Saudi Arabia umeahirishwa kwa mwaka mmoja zaidi.
Korir alitangaza hayo kupitia taarifa akisema kuwa makubaliano yaliafikiwa baada ya mazungumzo magumu kati ya misheni huko Riyadh, mamlaka ya Saudi Arabia na mamake Munyakho.
“Ninafuraha kujulisha kwamba baada ya mazungumzo magumu kati ya Misheni yetu huko Riyadh, Mamlaka za Saudia na Mjane, utekelezaji wa hukumu dhidi ya Stephen Munyakho (Abdulkareem) uliotarajiwa Novemba 26, 2024, umeahirishwa kwa mwaka mwingine mmoja ili kuruhusu pande zote kutatua majukumu yaliyosalia,” alisema.
“Tutaendelea kutegemea uhusiano mzuri wa nchi zetu mbili katika kuhitimisha suala hili. Nia njema ya Wakenya wote, washirika, na washikadau inathaminiwa kwa usawa. Nampongeza Balozi Ruwange kwa uongozi wake katika jambo hili muhimu.”
Stephen, ambaye amefungwa kwa miaka 13, mwanzoni aliratibiwa kunyongwa Mei 15, 2024. Hata hivyo, wenye mamlaka waliongeza muda hadi Julai 26, 2024, kisha ikaahirisha kwa miezi minne hadi Novemba 26, 2024.
Munyakho alipatikana na hatia ya kumuua raia wa Yemen nchini Saudi Arabia mnamo Aprili 2011. Akiwa meneja wa ghala, Munyakho alipigana na Abdul Halim Mujahid Markad Saleh, ambaye familia yake bado inaishi Saudi Arabia.
Wakati wa ugomvi huo, Stephen alimchoma kisu Abdul kwenye paja na kidole gumba. Baadaye Abdul alitembea hadi hospitali ambapo alifariki dunia.
Kufuatia tukio hilo, Munyakho alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la mauaji. Hata hivyo, familia ya Yemeni ilikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo katika Mahakama ya Shariah, ikitumia ‘haki ya kulipiza kisasi’.
Awali, Munyakho alihukumiwa kifungo kwa kuua bila kukusudia. Kufuatia rufaa ya familia ya marehemu, mashtaka yalipadilishwa na kuwa mauaji ambapo hukumu ni kifo.
Mnamo mwaka wa 2014, mahakama ilibatilisha hukumu ya awali ya miaka mitano na kutoa hukumu ya kifo kwa upanga. Baada ya mazungumzo, familia ya mwathiriwa ilikubali kupokea Diya, au pesa za damu, kama fidia chini ya sheria ya Kiislamu. Kiasi cha awali kiliwekwa kuwa Riyal za Saudi Arabia (SAR) milioni 10, sawa na Ksh 400 milioni.
Mazungumzo zaidi kati ya familia hizo yalipunguza pesa za damu hadi SAR milioni 3.5, sawa na Ksh 150 milioni wakati huo ambazo lazima zilipwe kabla ya Munyakho kuachiliwa.