Saa za Swatch zapigwa marufuku nchini Malaysia

Marion Bosire
2 Min Read

Saa zilizoundwa na kampuni ya Swatch ambazo rangi zake ni za upinde wa mvua na uhusishwa na kundi la mashoga, wasagaji na wengine almaarufu LGBTQ zimepigwa marufuku nchini Malaysia.

Yeyote atakayepatikana akiagiza saa hizo, kuuza au kuzivalia atakabiliwa na kifungo cha miaka mitatu gerezani na kutozwa faini ya dola 4,310.

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Malaysia ilitoa taarifa ambapo ilielezea kwamba saa hizo zina madhara au huenda zikawa na madhara kwa maadili, maslahi ya umma na maslahi ya kitaifa kwa kutangaza, kusaidia na kuhalalisha kundi la LGBTQ ambalo halikubaliki nchini humo.

Ushoga umepigwa marufuku nchini Malaysia na watakaopatikana wakijihusisha na mapenzi ya jinsia moja wanakabiliwa na adhabu ya faini na kifungo cha hadi miaka 20 gerezani.

Malaysia pia ni mojawapo ya nchi 13 ulimwenguni ambazo zimeharamisha kabisa utambulisho wa watu ambao wamebadili jinsia.

Tangazo la kupiga marufuku saa za Swatch za rangi za mashoga nchini Malaysia linafuatia hatua ya maafisa wa usalama nchini humo kuvamia maduka 11 ya Swatch mwezi Mei na kuchukua saa hizo zenye alama za mashoga za thamani ya dola elfu 14.

Tawi la Malaysia la kampuni ya Swatch liliwasilisha kesi katika mahakama kuu nchini humo kupinga uvamizi huo na kuchukuliwa kwa mali yake.

Wamiliki wa kampuni hiyo wanasema hawaelewi ni kwa nini serikali inapinga saa zilizoundwa kwa rangi za upinde wa mvua ambao ni asilia.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *