Ruto: Wakulima milioni 6.4 wamegawiwa mbolea ya bei nafuu

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto

Jumla ya wakulima milioni 6.45 wamegawiwa mbolea ya bei nafuu tangu mwezi Februari mwaka huu katika hatua ambayo imeboresha mno mazao yao. 

Rais William Ruto anasema wakulima hao ni wa kutoka 45 kati ya kaunti zote 47 nchini.

Katika hotuba yake kwa taifa katika Bunge la Taifa leo Alhamisi, Rais Ruto amesema mwaka huu, serikali imesambaza magunia milioni 7 ya mbolea kwa wakulima ili kuboresha uzalishaji wa chakula nchini.

“Hatua hii itasababisha ongezeko la uzalishaji wa mahindi kufikia magunia milioni 74 ya kilo 90 ambayo ni rekodi,” amesema Ruto.

“Pia tumefikia makubaliano ya muda mrefu na wasambazaji 11 ya usambazaji mbolea ili kuhakikisha bidhaa hii inapatikana mwaka mzima.”

Kulingana na Rais, mbolea ya msimu wa mvua ndefu itahifadhiwa kwenye ghala kote nchini katika hatua mbayo itahakikisha wakulima wanakuwa tayari kwa shughuli za upanzi.

Ameelezea matumaini kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali zitahakikisha nchi hii ina chakula cha kutosha kukidhi mahitaji yake. Hii itasaidia kupunguza gharama kubwa zinazotokana na uagizaji wa chakula ughaibuni.

Kutokana na juhudi za serikali, Rais amesema kwa sasa Kenya ina magunia milioni 47 ya mahindi ya kilo 90, magunia milioni 8.8 ya maharage, magunia milioni 10.4 ya mtama na magunia milioni 2.1 ya mchele.

 

 

Share This Article