Rais William Ruto ameelezea namna Kenya inavyothamini mno uhusiano wake wa kidiplomasia na China.
Amesema uhusiano kati ya nchi hizo mbili hususan umejikita kwa heshima ya pande mbili, ushirikiano wa kimkakati na malengo ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na uthabiti wa kikanda.
“Ushirikiano huu unadhihirishwa na mipango ya pamoja inayotekelezwa chini ya Mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja, inayoangazia miradi ya miundombinu, biashara na teknolojia ambayo inaunga mkono maono ya ukuaji na usasa ya Kenya.”
Rais Ruto aliyasema hayo leo Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi alipofanya mazungumzo na Li Xi, mwanachama wa Kamati Simamizi ya Ofisi ya Kisiasa na Katibu wa Tume Kuu ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).
Ruto aliwasihi raia wa China kuwekeza nchini Kenya hasa katika nyanja za nishati mbadala, kilimo na miundombinu ya dijitali ili kuimarisha ajenda ya mabadiliko ya taifa la Kenya.
Li aliwasili humu nchini Jumamosi iliyopita kwa ziara rasmi ya siku tatu.
Punde baada ya ndege yake kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA, Li alilakiwa na Kinara wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.
Aidha Li anatarajiwa pia kukutana na viongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kujadili njia za kuimarisha ushirikiano kati ya CPC na UDA kwa lengo la kuimarisha huduma zinazotolewa na vyama hivyo vya kisiasa kwa raia.
Ziara yake imewadia wiki chache tu baada ya mkutano wa ushirikiano kati ya China na Afrika kukamilika nchini China.