Ruto – Nibandikeni majina 10 yatoshane na ile miaka

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto sasa anaonekana kugeuza rundo la majina wanayombandika Wakenya kila uchao kujinadi kwao.

Akizungumza katika siku ya mwisho ya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika kaunti ya Nairobi leo Ijumaa, Rais Ruto amewataka Wakenya kumbandika hadi majina 10 ya utani kuwiana na miaka kumi anayosema atahudumia taifa kama Rais.

“Majina ni mingi. Lakini kazi mimi nitafanya, na ninataka kufanya mnaniongezea majina. Naendelea kufanya mnaniongezea majina. Mimi naona tuongeze mpaka ifike kumi, itoshane na ile miaka.”

Wakenya wamekuwa wakimbandika Rais Ruto majina mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zakayo, Kasongo, na la hivi karibuni ni El Chapo, jina alilobandikwa baada ya kuahidi kutoa mashine ya kutengeneza chapati milioni moja wakati wa ziara yake katika kaunti ya Nairobi wiki hii.

Aidha, wakati wa ziara yake katika maeneo mbalimbali ya kaunti ya Nairobi kama vile Makadara na Embakasi, Ruto alizungumzia ndoa yake ya kisiasa na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga akielezea kuwa ilinuia kumaliza zimwi la ukabila na siasa za chuki humu nchini.

“Ndio nimekubaliana na hata Raila Amollo Odinga, former Prime Minister, tumekubaliana na yeye ya kwamba hatutaki ukabila Kenya, hatutaki siasa ya chuki Kenya, hatutaki siasa ya migawanyiko Kenya, inaturudisha nyuma, inatugawanya, inaingiza chuki katika taifa letu la Kenya.”

Rais Ruto aliingia rasmi katika ndoa ya kisiasa na Raila Ijumaa wiki iliyopita.

Hii ina maana kwamba Raila hatagombea tena wadhifa wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Badala yake, kinara huyo wa ODM aliyetemwa siku chache zilizopita katika jitihada zake za kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ataunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto ambaye alikuwa mpinzani wake mkuu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka wamekosoa hatua ya Raila kuungana na Ruto wakiitaja kuwa usaliti na ya kujitakia makuu.

Kalonzo, na viongozi wengine wa upinzani kama vile Martha Karua, waliunga mkono azma ya Raila kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita, uchaguzi ambao alishindwa na Rais Ruto.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *