Kenya na Morocco zinaendelea kuboresha ushirikiano, asema waziri Joho

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri Hassan Joho (Kushoto) na Waziri wa Uchukuzi wa Morocco Abdessamad Kayouh.

Kenya na Morocco zimethibitisha kujitolea kwao kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili katika sekta za baharini, uchukuzi na usafirishaji.

Waziri wa Madini na Uchumi wa shughuli za baharini Hassan Joho alisema ahadi hiyo mpya inafuatia mkutano baina yake na Waziri wa Uchukuzi wa Morocco Abdessamad Kayouh huko Rabat.

“Tulijadili ushirikiano baina ya Kenya na Morocco, hususana kuhusu maswala ya baharini, uchukuzi na uunganishwaji,” alisema waziri Joho kwenye ukurasa wake wa X.

Kulingana na Joho, pia waliangazia ushiriki wa Kenya na Morocco katika Shirika la Kimataifa la Baharini (IMO), ambapo nchi hizo mbili zinalenga kuimarisha majukumu yao katika kubuni sera ya baharini ya kimataifa.

Waziri huyo alisema Kenya inatambua juhudi za kupigiwa mfano za Morocco katika Baraza la IMO chini ya kiwango cha C na inathibitisha tena kuunga mkono azma ya Morocco ya kusalia katika baraza hilo.

Joho alifichua kwamba Morocco pia ilikuwa imeihakikishia Kenya uungwaji mkono wake katika azma yake ya kuchaguliwa tena katika kiwango hicho katika IMO hatua inayoashiria kuongezeka kwa ushirikiano wa baharini na usaidizi kati ya mataifa hayo mawili.

Waziri huyo alikuwa ameandamana na balozi wa Kenya nchini Morocco Jessica Gakinya miongoni mwa maafisa wengine wakuu wa serikali.

Website |  + posts
Share This Article