Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiza kesi za kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Rais William Ruto anasema ni Mahakama ya Upeo pekee iliyotwikwa mamlaka hiyo.
Ruto kupitia wakili wake Adrian Kamotho sasa anataka Mahakama Kuu kuacha kusikiza kesi hizo na badala yake kuzielekeza kwa Mahakama ya Upeo.
Kulingana naye, Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiza kesi zinaohusiana na masuala ya uchaguzi.
Anapinga kesi iliyowasilishwa na David Mathenge na watu wengine wanne katika Mahakama ya Kerugoya Law Courts, ambako agizo la kuzuia kwa muda kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki lilitolewa.
Awali, wanasheria wa pande zote katika kesi hiyo kutifua kivumbi cha sheria juu ya faili zilizo mbele ya jopo la majaji watatu wanaosikiza kesi hiyo.
Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Eric Ogola, Anthony Mrima na Freda Mugambi liliteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome kusikiza kesi hiyo.
Wanasheria wa Gachagua wametilia shaka kubuniwa kwa jopo hilo Jumamosi iliyopita kusikiza kesi kesi hizo.
Gachagua alikuwa amewasilisha kesi zipatazo 20 kupinga kubanduliwa kwake madarakani, kesi ambazo mahakama ilizijumuisha pamoja.
Hususan, wanasheria wa Gachagua walitaka kubaini ikiwa faili ya kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya Kerugoya imewasilishwa mbele ya jopo hilo.
Katika agizo lake, mahakama ya Kerugoya ilizuia kuapishwa kwa Naibu Rais mteule.
Majaji hao waliwataarifu kuwa faili hiyo haijawasilishwa kwao.