Ruto aurushia upinzani makombora, asema hauna ajenda

Rais amesema wananchi hawataki kujua namna viongozi wa upinzani wanavyopangana, bali wanavyowapanga.

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto amehusisha migawanyiko iliyokithiri katika mrengo wa upinzani na kukosa ajenda yenye manufaa kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo la Kisii leo Jumatatu, Ruto amesema hababaishwi kamwe na atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya mrengo huo katika uchaguzi wa urais mwakani.

“Kuna watu wengine hapo wanatuletea makelele mingi, sijui kila asubuhi, wanatuambia bado tuko pamoja. Kila asubuhi, bado hatujasambaratika, oooh tutaleta candidate moja, sijui tutaleta candidate ngapi. Sasa mimi nataka niwaulize nyinyi majamaa, for the last one and half years, mnatupatia story, ati mtakuwa candidate moja, sijui hamjasambaratika, sijui bado mko pamoja, nani aliwauliza?” Ruto alisema wakati akiupuuzilia mbali upinzani.

“Wananchi hawa wa Kenya wanataka kujua mpango yao. Wananchi hawa wanataka kujua maisha yao itabadilika namna gani? Wanataka kujua, kilimo yao itaweka pesa kwa mfuko kwa njia gani? Watoto wao watasoma kwa njia gani? Barabara yao itajengwa kwa njia gani? Matibabu yao itafika kwa njia gani? Hiyo ndio hawa wananchi wanataka kujua.”

Ruto aliumiminia upinzani mashambulizi wakati ambapo kumeonekana kutokea nyufa miongoni mwa viongozi wa upinzani kiasi kwamba kinara wa DCP Rigathi Gachagua amewalaumu baadhi yao kwa kuzembea badala ya kufanya kampeni kali za kumbandua Ruto madarakani.

Aidha, haijabainika wazi atakayepeprusha bendera ya kugombea urais ya mrengo huo wakati Gachagua, kinara wa Linda Mwananchi Edwin Sifuna, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Dkt. Fred Matiang’i wa Jubilee, wote wakimezea mate wadhifa huo.

 

Share This Article